WELCOME TO THE REPUTABLE BLOG IN TOWN WITH FANTASTIC NEWS,GOSSIP,TALENTS,FASHION,MOVIE STAY ON THIS WEBSITE
RSS

FURAHA KWA WATANZANIA BAADA YA KUMALIZIKA KWA MGOMO WA MADAKTARI!

Veronica Lawrence, mama wa mtoto wa miezi mitano, Suleiman Abdallah, akionesha utumbo wa mwanawe uliotokeza nje akiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam Ijumaa kufuatilia matibabu. Tundu hilo ndipo inapotokea haja kubwa ikichanganyika na damu na alishawahi kulazwa hospitalini hapo kwa takribani miezi miwili na bado hajapata nafuu. SIKU moja baada ya kumalizika kwa mgomo, madaktari katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili
na zingine za umma nchini, wamerejea kazini.

Akizungumza na 'HabariLeo' jana, mmoja wa viongozi wa Kamati ya Kufuatilia Madai ya Madaktari, Dk. Frank Kagoro, alisema wamerejea kazini bila kinyongo. Alisema ingawa mazungumzo yao na Waziri Mkuu hayakutoa majibu ya matatizo yao yote, lakini wameamua kurejea kazini ili kuridhia makubaliano hayo.


“Ingawa hatukuridhika na baadhi ya maelezo ya Waziri Mkuu, tumekubali kurudi kazini na kuchapa kazi kwa bidii, kwa sababu Serikali imeonesha nia ya kukaa meza ya mazungumzo, kutusikiliza na kutafutia ufumbuzi wa matatizo yanayotukabili,” alisema Dk. Kagoro.


Alisema madaktari hao watatumia nafasi waliyopewa ya kutoa mapendekezo mapya kwa kugusia pia mambo ambayo hayajawaridhisha na kisha kuyawasilisha kwenye Tume iliyoundwa kwa lengo la kuchunguza na kutoa mapendekezo kuhusu kero zao. Alisema kwa kuwa madaktari walipewa fursa ya kuendelea kukutana na viongozi wa Serikali kwa ajili ya kushughulikia matatizo yao, wamepanga kufanya mkutano huo Machi 3.


“Mkutano huo ndio utakaokuwa na majibu sahihi kama madaktari wameridhika au la, lakini la muhimu zaidi tunaiomba Serikali itimize tuliyokubaliana,” alisema Dk. Kagoro. Madaktari walirudi kazini jana baada ya kufanya mgomo uliodumu takribani mwezi mmoja kwa lengo la kuishinikiza Serikali kutekeleza madai yao.


Mgomo huo ulimalizika juzi baada ya Waziri Mkuu Pinda kukutana nao Muhimbili ambapo pamoja na mambo mengine, alitangaza kuwasimamisha kazi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Deo Mtasiwa.


Alisema Blandina na Mtasiwa wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili na madai kwamba wamekuwa kiini cha matatizo kilichosababisha madaktari

hao kugoma. Pia Waziri Mkuu alikubali kushughulikia mapendekezo manane yaliyotolewa na madaktari hao.

Kuhusu Waziri Dk Haji Mponda na Naibu wake, Lucy Nkya, Waziri Mkuu alisema watawajibishwa na Rais. Miongoni mwa matakwa ya madaktari hao ili kusitisha mgomo ilikuwa ni kuondolewa kwa viongozi hao wanne katika wizara hiyo, ambayo pia Pinda alisema kuna matatizo na hivyo kuwapo haja ya kuisafisha.


Mbeya


Kutoka Mbeya, Joachim Nyambo anaripoti, kwamba hali ya utoaji wa matibabu katika Hospitali ya Rufaa Mbeya jana ilirejea kawaida japo kwa kuchelewa, kutokana na madaktari kuanza shughuli yao kwa kikao na baadaye wakaanza kutoa huduma.


'Habarileo' lilitembelea hospitalini hapo saa nne asubuhi na kukuta huduma zikiendelea kama kawaida huku waganga na wagonjwa wakiitupia lawama Serikali kwa kuchelewa kulipatia ufumbuzi suala la mgomo huo. Mmoja wa madaktari, Dk. Saliji Manyaka, alikiri kuendelea kutoa huduma akisema hatua iliyofikiwa ni nzuri na kutoa ahadi kwa wagonjwa kuwa watarajie kupata huduma nzuri ya tiba.


Dk. Benedict Nkuwi alisema tukio la mgomo uliomalizika linapaswa kuwa somo la kuhakikisha migogoro inamalizwa kabla haijaleta athari kubwa kwa jamii. Hata hivyo, aliwashangaa wanaoitupia lawama Serikali, akisema wanajisahau kuwa wao pia ni sehemu ya Serikali hivyo kinachotakiwa ni kuwabana wanaowawakilisha katika uongozi kuhakikisha wanakuwa na mipango madhubuti.


“Watu wanasema Serikali haifanyi, lakini wanajisahau kuwa sisi ndiyo Serikali. Wale tumewaweka kwa kuwa hatuwezi tukawa viongozi wote. Hivyo hili ni fundisho kwetu sote tunaoiunda Serikali, kuwa tunapaswa kujenga mazingira ya kutatua migogoro kabla haijaleta madhara makubwa,” alisema.


Mmoja wa wagonjwa hospitalini hapo, James Manyanya, kutoka Mpanda mkoani Rukwa, alisema kabla ya kufika hospitalini, alikuwa na hofu kutokana na mgomo uliokuwa unaendelea, lakini kwa bahati nzuri alifika mgomo ukiwa umemalizika.


Katika hatua nyingine, Regina Kumba anaripoti kutoka Mahakama ya Kisutu, kwamba Umoja wa Wazazi wa Kiislamu Tanzania umefungua kesi ya madai katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam dhidi ya madaktari, ukiitaka Mahakama kutamka kuwa mgomo wa madaktari wa zaidi ya wiki mbili ni kinyume cha sheria.


Aidha, katika kesi hiyo ya madai iliyofunguliwa mwishoni mwa wiki na kupewa namba 13 ya mwaka huu, iliambatanishwa na maombi yaliyopewa namba hiyo hiyo.



  • Digg
  • Del.icio.us
  • StumbleUpon
  • Reddit
  • RSS

0 maoni: