Waziri Mkuu Mstaafu Bw. Edward Lowassa akizungumza na waandishi wa
habari (hawapo pichani) Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere
(JNIA) Dar es Salaam jana, mara baada ya kurejea nchini kutoka nchini
Ujerumani alikokwenda kufanyiwa uchunguzi wa macho, kushoto ni Mke wake
Bi. Regina Lowassa. (Picha na Prona Mumwi)
Na Rachel Balama WAZIRI Mkuu aliyejiuzulu Bw.
Edward Lowassa, amerejea nchini jana alasiri akitokea nchini Ujerumani
alipokuwa kwa matibabu na kutamba kuwa, afya yake ipo imara na yupo
tayari kwa mapambano.
Bw. Lowassa aliyasema hayo Dar es Salaam
jana wakati akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya
kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).
Alisema
taarifa mbalimbali zilizokuwa zikisambazwa kuwa afya yake si nzuri na
amepata kiharusi si za kweli, zimemsikitisha na kumshangaza sana.
“Nimerudi
salama, nipo fiti zaidi hivyo nitaendeleza mapambano,” alisema Bw.
Lowassa na kuongeza kuwa, mapigo yake ya mayo yapo safi kwa kiwango cha
120 chini ya 80.
Hata hivyo Bw. Lowassa hakuwa tayari kufafanua
mapambano ambayo atayaendeleza. Alipoulizwa kwanini anazushiwa ugonjwa
wa kiharusi alijibu kwa mkato “kawaulizeni wenyewe”.
“Huo ni
uongo wa kutupwa, niliondoka nchini nikiwa na afya nzuri nikitembea
mwenyewe...nimeshangaa kusikia taarifa za uwongo kuwa afya yangu si
nzuri, eti nilikuwa hoi,” alisema Bw. Lowassa.
Alisema miaka
mitatu iliyopita, alifanyiwa upasuaji wa macho nchini Ujerumani na
kuanzia hapo daktari wake alimshauri kila baada ya miezi sita awe
anarudi nchini humo kuangalia maendeleo.
Alisema daktari wake amemwambia hali yake inaendelea vizuri hivyo haitaji kufanyiwa tena upasuaji.
Bw.
Lowassa ambaye alionekana kukwepa maswali mengi aliyokuwa akiulizwa
hasa ya kisiasa, hakuwa tayari kufafanua kama atakwenda kushiriki
kampeni za uchaguzi mdogo Jimbo la Arumeru Mashariki, mkoani Arusha.
“Sijui
kama nitashiriki, hata nikienda tutakutana huko huko, nawashukuru watu
wote walioniombea na wale walionijulia hali nikiwa Ujerumani katika
matibabu,” alisema.
Kwa upande wake, mkewe Bi. Regina Lowassa
alipoulizwa kama mume wake yupo fiti na anaweza kuendelea na mapambano
alikiri yupo fiti na anaendelea vizuri.
Wakati huo huo,
Mwandishi Willbroad Mathias anaripoti kuwa, baada ya mvutano wa mrefu
kuhusu urejeshwaji wa chenji ya rada, hatimaye Tanzania itaweza
kurejeshewa fedha hizo pamoja na riba ili zitumike kwa ajili ya
kuboresha sekta ya elimu.
Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana
kwa vyombo vya habari na Mshauri wa Habari kutoka Idara ya Maendeleo ya
Kimatifa (DFID), Bi. Eunice Urio, alisema hatua hiyo imefikiwa baada ya
kusainiwa Mkataba wa Makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania, Kampuni
ya Kuuza Vifaa vya Kijeshi-BAE Systems na Ofisi ya Kupambana na Ufisadi
nchini Uingereza (SFO).
Bi. Urio alisema kutokana na makubaliano
yaliyofikiwa jana, Kampuni ya BAE Systems itarejesha fedha hizo katika
Benki Kuu ya Tanzania kitita cha pauni milioni 29 pamoja na riba kama
ilivyofikiwa katika makubaliano.
Aliongeza kuwa, tayari Serikali
ya Uingereza na Tanzania zimefanya kazi bega kwa bega ili kuamua fedha
hizo zitumike kwa ajili ya kitu gani na jinsi zitakavyofuatiliwa.
“Lengo
ni kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa ambayo ni kuboresha sekta ya
elimu yanafikiwa, katika makubaliano fedha hizi zitatumika kununulia
vitabu kwa ajili ya shule 16,000 za msingi.
“Wanafunzi milioni
8.3 watanufaika na vitabu hivi ambavyo vitakidhi masomo yote 11 kuanzia
darasa la kwanza hadi la saba, kipaumbele kitatolewa kwa masomo muhimu
ya Kiswahili, Kiingereza, Hisabati na Sayansi,” imesema taarifa hiyo.
Imeongeza
kuwa, wanafunzi wawili watatumia kitabu kimoja lakini idadi kamili ya
vitabu ambavyo vitanunuliwa bado inajadiliwa na kusisitiza makubaliano
hayo hayatawekwa hadharani hadi mchakato wa manunuzi utakapokamilika Mei
mwaka huu.
Bi. Urio alisema mbali na kununua vitabu pia kiasi
fulani cha fedha kitaelekezwa kwa walimu 175,000 ili kuwajengea uwezo
ambapo zaidi ya dola za Marekani milioni tano zitaelekezwa katika
ununuzi wa madawati |
0 maoni:
Post a Comment